Pages

Friday, 13 June 2014

NAMNA YA KUPATA MWENZI ANAYEKUFAA MAISHANI( PR MWANGA)


NAMNA YA KUPATA MWENZI ANAYEKUFAA MAISHANI

Ndoa iliyo bora na furaha tele haianzi hewani bali ina msingi wake. Furaha siyo kitu cha kupata kama bahati nasibu. Ni jambo ambalo unajenga kama mtu ajengavyo nyumba imara. Lazima aweke msingi ambao utafanya nyumba idumu au ianguke. Hivyo kijana wa kiume na wa kike picha halisi ya ndoa bora na yenye amani inafanyika wakati wa uchaguzi wako wa kupata mwenzi wa maisha yako. Uchaguzi wowote na namna ulivyofanyika utaamua hatima ya aina ya ndoa uitakayo. Zipo kanuni chache tutakazoziangalia kwa vijana wa kike na kiume namna wanavyoweza kupata mwenzi atakayewapa furaha na amani tele katika nyumba zao badala ya majuto na huzuni. Na pia kuondoa kauli laiti ningejua au najuta kuolewa na mwanaume huyu ama kumuoa mwanamke huyu.

MVULANA UTAMPATAJE MSICHANA ATAKAYEKUWA MWENZI ANAYEFAA
Zipo kanuni za msingi ambazo kama kijana wa kiume unaweza kufanya katika uchaguzi wako. Hebu twende hatua kwa hatua katika swala hili:
  1. Kijana mpatie Yesu maisha yako kwa asilimia 100. Jitoe kwa Yesu ili akupe mke mwema. Kumbuka mke mwema hutoka kwa Bwana. MITHALI 31:10.
  2. Maombi ndio silaha na dira itakayokuonyesha chaguo lako. Orodhesha sifa za binti umtakaye awe mwenzi wako. Huenda awe msomi, mfanyakazi, mkulima, mtu wa kiroho, mkarimu, na kadhalika. MWANZO Kisa cha Isaka na Rebeka.
  3. Fanya uchaguzi wa mchumba. Kisha anza kujenga urafiki na pia fanya uchunguzi wa mwenendo wa maisha yake ili upate dalili uzitakazo. Hapa usiharikishe kumtakia kuwa utamuoa maana ataficha makucha yake.
  4. Fanya liwe ni jambo la lazima kuoana na mtu wa imani moja na wewe. Usikubali kuoana na mtu ambaye siyo wa imani moja na wewe. Mkatoliki awe mkatoliki. Mwislamu hali kadhalika. Epuka kugawa watoto na kuondoa furaha na umoja wa familia. Na hata kushindana katika mambo ya imani.
  5. Chukua muda wa kutosha kujifunza tabia yake. Usiharakishe kumuoa bila kujifunza tabia yake. Uchumba wenu usipungue miezi sita na kuendelea. Upande wa pili usizidi sana miaka minne. Muda mfupi haukupatia nafasi ya kujua madhaifu yake na mazuri yake. Muda mrefu nao unaleta mashaka na kujaribiwa kwa mwenzi wako anapoona miaka inasonga hasa mwanamke.
  6. Oana na mwanamke ambaye tabia zenu zinafanana ama kulingana au kuendana. Kama ni mkulima basi usitafute binti wa ofisini yatakushinda.
  7. Kijana epuka kuoa maumbile ya mwanamke (physical appearance). Wengi wanajutia kwani hakujua mwili huwa unachujuka wakati mwanamke anapoolewa aidha kwa kuzaa ama kukabaliana na changamoto za ndoa. Miguu ya bia huwa inabadilika na kuwa ya Coca Cola. Namba nane huwa namba moja.
  8. Usifanye uchaguzi wa sura pekee kama kiini cha chaguo lake. Bali tabia iwe ndicho kiini cha kwanza na sura iwe namba pili. Ni kweli ni vizuri ukaoa mwanamke ambaye ana sura nzuri hata ukitembea barabara unafahari kwenda naye. Siyo ambaye unaona haya kumtambulisha kama mkeo. Lakini sura ikiwa ndicho kiini utaishia kwenye majuta kila siku maana visura wengi bado hawajazaliwa.
  9. Unapopata msichana tafuta ushauri wa watu wenye heshima wanaomfahamu vizuri. Wanaweza kuwa wachungaji, masheikh, wazee au watu wa makamo. 
  10. Epuka msichana mwenye tamaa vitu. Msichana anayekuomba mara hiki au kile huyo atakusumbua mapema.
  11. Jaribu kujua habari za marafiki wa karibu sana wa Yule msichana. Utakapoona na wale ambao hapo mtaani wanasifika kwa tabia mbaya ni dalili mbaya kwa mahusiano yako na yake. Hapa unaweza kumpima kwa kutoka naye out’utakapoona anasimamishwa kila kona tambua kuwa huyo ni jamvi la wageni. Msichana anayejiheshimu huwezi kusimamishwa njia yote na wanaume.
  12. Mwisho: Unapogundua mapungufu ambayo huyapendi ni bora kuvunja uchumba kuliko kuvunja ndoa. Tambua huwezi kumbadilisha mtu tabia yake. JASIRI HAACHI ASILI!

MSICHANA UTAPATAJE MVULANA ANAYEKUFAA MAISHANI MWAKO
Kazi ya ziada kwa msichana kujua mvulana ambaye ni wa kweli. Kwani ni vigumu sana kwa wasichana wengi kujifunza tabia ya kijana wa kiume kwa makini sana. Wasichana wanaona haya kuuliza habari za mvulana Fulani kwa watu kwani wanaogopwa kuulizwa unataka nini kwake. Lakini yapo mambo ya muhimu sana ambayo msichana unaweza kufanya ili kupata mwenzi ambaye atakupa furaha ya kweli katika ndoa yako. Kumbuka mwanamke nawe unauchaguzi wa kufanya. Fanya mambo yafuatayo:
  1. Msichana jitoe maisha yako kwa Yesu kwa asilimia zote ili Bwana akupatie kilicho bora maishani mwako. MITHALI 16:7
  2. Msichana jiheshimu sana mbele za watu na hata uwe mwaminifu mbele ya jamii unayoishi.
  3. Weka swala hili katika maombi na pia weka sifa Fulani ambazo unazitaka kutoka kwa Mungu kwa mwenzi atakayekupatia. Sifa ya kwanza ombea upate mcha Mungu.
  4. Usikatishwe tamaa unapoona vijana wengi hawakufuati. Tulia maana siku zote mambo mazuri hayana haraka. Usipayuke yuke kuwa mbona huolewi.
  5. Chagua mwanaume anayependa kazi. Usibague kazi anayofanya alimradi ni mtu mwenye bidii acha kuangalia uzuri wa kazi yake. Mwenye bidii anaweza kubadilisha maisha katika hali yeyote wakati wowote.
  6. Usikubali kwa gharama iwayo yote kuolewa na mtu ambaye hapendi kazi. Epuka kugeuzwe kuwa kiwanda cha watoto na kuzalishia mali. Epuka kulala njaa na watoto. Ukiolewa na mvuvi nyumba yake itakuwa na taabu nyingi na umasikini mwingi.
  7. Jenga urafiki na wavulana wote kwa heshima. Usibague wavulana wa kuzungumza nao. Wanaume wengi wanaogopwa kudharauliwa na kuaibishwa na wanawake.
  8. Epuka kama ukoma kuolewa mtu asiyeamini au mtu asiye wa imani moja na wewe. Ni vigumu sana kwa wanaume kubadilisha dini yake.
  9. Olewa na mtu mnayefanana tabia zenu. Kama ni mlevi basi olewa na mlevi mwenzako au mvuta sigara mwenzake ili starehe ya  mwingine isiwe kero ya mwingine. Ijapokuwa nyumba ya mlevi kumbuka haina amani. MITHALI 20:1; 23:30 – 35.
  10. Msichana inakupasa uwe ni mtu wa gharama kubwa. Jiweke katika kiwango cha juu hata kama unatoka katika familia masikini. Usikubali kupewa zawadi ovyo ovyo. Kumbuka kila zawadi inayotolewa na mwanaume utailipa.
  11. Usikubali kuolewa na mali au fedha au umaarufu wa mtu. Kumbuka ikiwa utakuwa umefuata hivyo vitu huwa vinayeyuka na matokeo yake upendo wako utayeyuka pia maana ndivyo ulivyofuata hapo. Ni bora kuolewa na masikini anayempenda Mungu kuliko tajiri ambaye hana hofu ya Mungu atakuletea wanawake wengine.
  12. Msichana ni sumu kwa kufanya mapenzi na mvulana unayetaka awe mume wako. Jambo hili litaondoa uaminifu katika ndoa yako na kisha kutakuwa na tabia ya kutokuaminiana siku zote. Ikiwa anakuambia mpaka mfanye kitendo hicho ndipo akuoe ni bora ukavunja uchumba maana kijana huyo sio Mwaminifu kabisa. 

NDOA TAJIRI KUPITA ZOTE ZILIZOWAHI KUFUNGWA

NAMSHUKURU MUNGU KWA AJILI YA SIKU YA LEO NINAPENDA KUWEKA MASOMO HAYA YA PEKEE KUTOKA KWA PASTOR MWANGA AMBAYO MIMI BINAFSI YAMENIBARIKI SANA.UBARIKIWE UNAOENDELEA KUWAALIKA WENZAKO WASOME



NDOA TAJIRI KUPITA ZOTE ZILIZOWAHI KUFUNGWA  

 Mungu Mwana – YESU KRISTO ndiye aliyeanza kufunga ndoa ya kwanza. Ndoa iliasisiwa kwa njia ya muujiza wa ajabu! Wakati Yesu alipomuoperate Eva. Hata bado Yesu alionyesha heshima ya ndoa kwa kuhudhuria karamu ya harusi. Ajabu ya Hakika – muujiza wa kwanza tena kwa mwanadamu aliofanya Yesu alianzia pale Kana ya Galilaya kwa kugeuza maji kuwa divai. YOHANA 2:1-5. Ndoa ya fahari na tajiri ambayo imeshawahi kufungwa ni ile ya kana ya Galilaya ilifanikiwa kumwalika Yesu. Na wala sio Clinton bali mfalme wa wafalme. Hawakupungikiwa chochote. Hata ijapokuwa maarusi walikuwa maskini lakini kwa kuhudhuria Yesu – tajiri mkuu ilikuwa tajiri kupita zote.
-          Kwanini Yesu alifanya miujiza katika matukio haya ya ndoa? Ndoa ilikwisha poteza thamani yake kama alivyoasisi. Heshima, upendo, furaha, utii, n.k. vilitoweka ndani ya ndoa na kilichobaki unyama, mauaji, chuki, magomvi, n.k. Mwanaume kumkata mapanga mkewe bila hofu.
-          Fundisho la Yesu pale Kana ya Galilaya ni kuwa ndoa na Yesu havitenganishiki. Anapoingia ubia maisha yanakuwa matamu kama divai iliyochujwa sana katika urojourojo wake tena ni mbaraka. Pale Edeni alifanya muujiza akijua ndoa itaingia shidani, mponyaji wa kweli wa ndoa sio mahakama wala wazazi au marafiki wala vikao vya kata. Hivyo ndoa na Yesu ni amani, furaha, na pia bubujiko la maji ya uzima.
Kicheko cha furaha kinaletwa na kitu kinachoitwa UPENDO WA KRISTO. Kabla sijazungumzia neno upendo hebu tuelewe maana ya ndoa: EBRANIA 13:4 – Malazi yawe safi? Iheshimiwe na watu wote? Kwanini Mungu atamke maneno kama hayo?
Neno ndoa ni ‘marriage’ means BED. Kiswahili ni kitanda. Mchungaji anapofungisha ndoa inamaanisha anatoa ruhusa ya kwenda kulala pamoja sio kama kaka na dada bali kufurahi mbaraka wa ndoa yaani tendo la ndoa. KISA CHA CHIBILA.  Hivyo mnapoolewa wana wa kike usifikiri mnaenda kuosha vyombo na kufua au kupika – acha! ILI NDOA IITWE NDOA NI MPAKA IWE NA UTAKATIFU WAKE KITANDANI.
-          Sio kanisa au serikali inayoweza kuita ndoa mahali ambapo match imefanyika na tena watu wamekula lakini hakuna kilichotendeka, moja kwa moja hiyo sio ndoa kisheria na kimbingu.
Biblia inaposema malazi yawe safi  - sio swala la usafi wa mashuka bali ina maana lazima kila mmoja awe mwaminifu kwa mwenzake – unapozini maana yake umeoa au umeolewa na mtu zaidi ya mmoja. Hili ndilo YESU anasema mwaweza kutengana tu kwa uasherati – uasherati maana yake uchafu. Mnapotoka nje ya ndoa hapo umechafua kitanda yaani ndoa yako. MITHALI 7:9-23. ; 6:26-29,32-33.
Biblia inaposema ndoa iheshimiwe ina maana kila mmoja ajali wajibu wake. Mume upendo na mke utii. Pia tambua unapooa mnaacha wapenzi wote na pia na wachumba wote kisha wazazi au mashemeji au mawifi hawana ubia hapo tena. Jihadhari usioe mke wa ukoo. Baba mkwe lazima aiheshimu ndoa yako sio apange masharti yake- hiyo ni serikali nyingine tayari.
ZINGATIA UPENDO – Upendo wa kweli haujengwi na fedha, nyumba, fedha, au mali bali YESU – IBADA. YESU AWE MFALME  - ASUBUHI, MCHANA NA JIONI. KISHA MUME AWE KIONGOZI TU SIO MTAWALA NA MKE AWE RAIA MWEMA.
Upendo sio kumuona mwenzako haendi kanisani na wewe unanyamazia .


Philosopher mmoja anayeitwa PLATO: Anasema ndoa ni kama ngazi yenye hatua za kupanda. Hatua ya kwanza ni kifungo cha UPENDO.
-          Hapa lazima umwambie mwenzako ulichompendea ili adumishe upendo. Kama ni unene au wembamba  eleza! KISA CHA MWANAMKE  mwembamba akala akawa mnene – matokeo ni kuachwa.
-          Hatua ya pili:- WATOTO – elewa watoto sio sio lazima ila wanapokuwepo ni mbaraka ambao umeongezewa. Maana mbaraka wa kwanza ni kupata mke au mume na kumuita wangu wakati ni mali ya MUNGU.  Watoto wanaongezea furaha lakini upendo kwanza. ZABURI 127:3. Kisa cha mtu aliyeng’ang’ania kupata mtoto lakini hakupata kisha akamwacha mke wake matokeo alioa mke na kupata watoto watano – wote ni mang’aa yaani balaa. Leo 2005 anakiri mbele za watu kuwa alimlazimisha Mungu na anajutia kuwa na watoto maana wote hawana faida zaidi ya kumtia huzuni! Fedheha! Aibu tupu !
-          Hatua ya tatu:- KAZI.  Kazi inaongeza furaha kila mmoja anapowajibika kwa juhudi. Inaondoa umaskini kisha inaleta furaha. Mama fanya kazi usiwe golikipa. Utaimarisha upendo. Kila mmoja afanye sehemu yake.
-          Hatua ya nne:- MWONEKANO WA NJE – PHYSICAL APPEARANCE. Kosa la wanandoa wengi ni kuoa sura. Ni kosa la hatari. Upendo wa kweli hauangalii katika vitu hivyo bali katika tabia safi. Kama tabia ni mbaya basi hata sura ikiwa nzuri kiasi gani, itakuwa mbaya wakati chuki inapoingia. Kumbuka visura ni wengi na bado hawajazaliwa. KOLOSAI 3:12 – 14.
-          Hatua ya Tano:- MAWASILIANO. – Hakuna upendo feki utakaojenga nyumba. Lazima mawasiliano yawe yameunganishwa kila wakati. Kama hakuna mawasiliano ndani ya nyumba hakuna faida ya kuishi pamoja. Upendo wa kweli unapatikana kwa mfalme wa Amani – YESU KRISTO MWASISI WA NDOA. Adamu alipomuona hawa kwa mara ya kwanza aliwasiliaana naye kwa tabasamu na shukrani tele. Angalia Paulo asemacho katika Wakolosai 3:15 – hiyo ndiyo ndoa ya kweli. Haya hayatanonekana ikiwa mawasiliano yamekatika au kuvunjika. MAWASILIANO NI UFUNGUO WA UTAJIRI KATIKA NDOA. Iwe ni raisi wa  nchi  ndani hakuna maelewano basi nchi yote inayumba. Au hakimu mahakamani – sheria yote inapotea. Mchungaji – mahubiri na mafungu hayaji. Kisa cha rubani wa ndege.
-           
ISHARA ZA MAWASILIANO KUKATIKA NDANI YA NDOA: UTAJUAJE?
UPANDE WA MWANAMKE:- MITHALI 5:15 – 18, 20 – 21. MUHUBIRI 7: 26 – 28.
Usiombe wewe mwanamume kukatiwa mawasiliano na mwanamke hasa anapokuwa ameunganisha mahali Fulani huko nje; hata kama ni maskini kiasi gani huyu mtu huwezi kumtoa utapiga ua HATOKI MTU!
  • Maji ya kuoga ni baridi wakati alikuwa analeta ya moto halafu sababu nyingi.
  • Chakula cha baridi kwa madai alipika saa nyingi wewe ndiwe umechelewa.
  • Unapomwita anaitikia mmh! Eeh! Unasemaje? Au anakuja tu.
  • Kuwa na madai mengi ya kusahau – kufua, kupasi, chakula, maji ya kuoga, n.k.
  • Majibu ya mkato – makazi yote haya umeona mi msukule, mi kainjini au tractor.
  • Tabasamu na kicheko hakuna. Lakini akija mgeni atachangamkiwa mpaka …..
  • Kuwa na hasira za mara kwa mara yaani kununa unapokuja au unapomsemesha.
  • Kutokutulia nyumbani kila saa kwa mashoga – amepata tuition ya mafiga matatu.
  • Kutokupokea unaporudi hakuna tena – anajifanya kama vile hajakuona na kwenda ndani ama kutokusindikiza unapotaka kusafiri. Utabeba begi lako mwenyewe mpaka...
  • Kutokufua nguo zako ama kupasi nguo mpaka umkumbushe ama ufue mwenyewe.
  • Kuchelewa akienda sokoni ama bombani na pia kuchelewa kupika kwa wakati ili uende na njaa kazini ama katika shughuli zako.
  • Kukulaumu kwa mambo mengi hasa nguo zake, ama chakula ama fedha unazompa anadai kidogo.
  • Kuficha simu yake inapoita anakwenda mbali ili kupokea simu yake kukwepa mume wake asijue. Ishara ya karibu sana ni pale simu hiyo inapomuhusu mpenzi wake atashituka. Simu yake hataiweka chini na hataki uwe nayo.
  • Mwisho salamu hakupatii tena, anaanza kwa kubip kwa magoti kama ni msukuma… hatimaye kubip kwa magoti hakupo tena kama ni kupiga magoti linaondolewa kabisa.

UPANDE WA MWANAUME:- MITHALI 15:17.
Wanaume ndio wanaoongoza kukata mawasiliano haraka katika ndoa. Hasa asiporidhishwa na msiba wake wa maisha yaani tendo la ndoa. Ndoa nyingi zinaharibika kwa sababu ya mambo yanayoanzia chumbani. Hivyo wachungaji na viongozi wa jamii wamekuwa wanatatua matawi badala ya shina lenyewe yaani tendo la ndoa,. Tofauti ya mwanaume na mwanamke ni kuwa mwanaume anapokata MAWASILIANO LAZIMA AUNGE HARAKA KWENYE MTANDAO MWINGINE. MWANAMKE KAMA NI BUZZ 0741 ATAHAMIA 0717. Lakini mwanaume lazima awe kwenye line wakati wote yaani BUZZ basi ataenda vodacom na celtel. Hivyo anakuwa na mitandao mingi maana anafanyia kazi mahali ambapo hakuna network.
  • Tabasamu na kicheko hakuna – ni ndita tu. Hili ni jambo la kwanza kila unapopiga simu “ the mobile number you are calling is busier the present; may you try again later.” – Tabasamu imehamia mahali fulani.
  • Mambo yake ni siri tu – mshahara wake, viwanja, mipango, n.k. wewe unapewa taarifa tu maana wewe ni housegirl tu.
  • Vizawadi hakuna tena. – kisa cha maua kwangu.
  • Kuchelewa kurudi nyumbani – kutopenda kuketi nyumbani masaa ya jioni bali kwenda kwa mtu au vijiweni.
  • Kufokafoka ovyo kwa watoto na mke na hata kwa wanyama – kuku, mbwa, paka, n.k.
  • Kutokula nyumbani bali kwa mama ntilie/ hotelini – kisa cha mama ntilie na mzee wa kanisa.
  • Kisha anaanza kupokea simu nje kama ni ndani ama mbali na mahali ulipo. Atakuwa mkali unaposhika simu yake. Hasa unaposoma message zake.
  • Hakuna salaam tena; na hata ukimsalimia ataitikia kwa ndani tu.
  •  Majibu ya mkato; haswa anapoishiwa fedha – mi kabenki, sawa! Haya! Tayari! Eeh! Nitakwenda. Nitanunua. N.k.
  • Kutokuamini mke wako. Ndo unarudi? Kwanini umechelewa? MITHALI 14:15.
  • Kukuita kwa dharau – wee mamaa nanihi. We mwanamke. Hebu niitie huyo.
  • Kudharau kila kazi unayofanya hakuna pongezi wala shukrani.
  • Hakuna mazungumzo yanayofanyika mpaka mgeni anapoingia – yametoweka.
  • Kunung’unika kwa jambo moja kwa muda mrefu. Kukulaumu mara kwa mara.
  • Madai ya kuumwa mgongo kila siku – hakuna tendo la ndoa kama kawaida.
  • Zingatia kwa makini ndoa tajiri kupita zote Suleimani anasema ni ya maskini mmoja aliye na YESU: “kula mboga za majani na upendo ni bora, kuliko ng’ombe aliyenona na magomvi” Yesu unapomwalika hakika ndoa yako itakuwa na mibaraka na nyumba yako amani tele. Hakuna upungufu wa divai wala hakuna magonjwa wala balaa bali furaha na kicheko cha furaha tele! 

Sunday, 1 June 2014

NAMNA MVULANA ANAVYOWEZA KUTAMBUA DALILI ZA MSICHANA ANAYEMTAKA KUISHI PAMOJA



NAMNA MVULANA ANAVYOWEZA KUTAMBUA DALILI ZA MSICHANA ANAYEMTAKA KUISHI PAMOJA.(Pr MWANGA)

“Somo hili ni muhimu sana kwa vijana wa kiume kutambua namna wanavyoweza kuitikia mwito kutoka upande wa pili wa wasichana. Wapo wasichana wengi ambao wanampenda mvulana Fulani na anatamani laiti angeliolewa naye. Lakini vijana wengi hilo hawalitambui na hata kama akilitambua anaanza kumfikiria vibaya yule binti kuwa ni mhuni au Malaya. Au pia anaamua kumtongoza kwa ajili ya mapenzi wakati hilo sio hitaji la binti. Mara nyingi wasichana wameangukia pua (pabaya) kwa kumkubalia mvulana wakifikiri hiyo ndio njia ya kuonyesha upendo zaidi kumbe matokeo yake wanaishi kutukanwa na kuchezewa na kudharaulika. Mwandishi mmoja aliandika hivi:  ‘inachukua dakika nzima kumpata mtu wa pekee katika maisha yako, na inachukua saa nzima kumkubali, inachukua siku nzima kumpenda lakini pia inachukua siku zote za maisha yako kumsahau”. – Mada hii nimenukuu kutoka katika mtandao. www.google.com
Wavulana wengi nao wameishia kuoa wanawake ambao kwa hakika hawawapendi lakini walichopendewa huenda umaarufu, kazi nzuri, fedha zake, au anataka katika familia ya kitajiri ama msichana amekosa aliyemtaka kwa hiyo anaolewa na huyo ili kumkomesha mvulana aliyemkataa. Ukweli wa mambo ndoa hiyo haitakuwa na mibaraka na furaha ya kweli bali huzuni kwa wakati mwingi maana hakuna upendo wa dhati. Sasa Mvulana utatambuaje kuwa msichana huyo anakupenda kwa dhati.
Zipo dalili za muhimu sana mvulana ataziona kutoka kwa msichana wa kweli.
  1. Ni binti ambaye anajiheshimu na pia akutanapo na wewe uso wake unaonyesha tabasamu la dhati.
  2. Macho ni dalili kubwa kupita zote. Maana anapokutazama anajisikia haya. Mtaalamu mmoja alisema “Macho ni dirisha la roho (nafsi).” Wapo wengine ambao macho yao kila wakati ataelekeza kwako kuonyesha umakini wa kukusikiliza wewe kuliko mtu yeyote. Mara nyingi atakuwa anakukodelea macho yako sio mahali popote. Kisha anakuwa na aibu nyingi kwako. Wavulana huwa wanaangalia wapi? Unajua!
  3. Mazungumzo yake kwako yanaonyesha heshima na tahadhari kubwa sana maana anakitu anataka ukione chema kutoka kwake. Anapenda kuzungumza mambo unayovutiwa nayo.
  4. Msichana anapenda kuwepo mahali ulipo kila wakati. Kama ni kanisa atataka benchi unalokaa liwe sambamba ama kikundi chako awepo. Ama safari zozote unazopanga kwenda naye hata kama hakutaka kwenda anakwenda. Tena anasema kama unaenda nami nitaenda. Hiyo ni dalili nzuri kabisa. Chuoni mwalimu anapowapa zoezi la kikundi atatafuta kukuangalia kwa sekunde chache ili kuonyesha muwe pamoja kwa zoezi hilo.
  5. Anakuwa ni msichana anayesikiliza mambo yako kwa makini na kutaka kujua mambo unayopendelea katika maisha. Huwa anapenda kuuliza maswali mengi yanayohusu maisha yako ya baadaye. Anakuwa na kumbukumbu za mambo yako mengi kuliko wewe. Anatamani kukuuliza kuwa unapendelea au vipi kuhusu jambo hili? Ujue ni ishara
  6. Lugha ya mwili:
i.                     Kuelekeza macho upande wako kila wakati,
ii.                  kutaka kushikana mikono kwa salamu ama anapocheka atataka kugongeana mkono na wewe ama kukushika mahali popote aidha kichwani au mabegani.
iii.                 Tabasamu kila mara akuonapo na kidevu chake kinang’aa kwa furaha.
iv.                kukutetea mara kwa mara unaposhutumiwa,
v.                  na anapogundua unapenda aina gani ya rangi za nguo au nywele atafanya kama upendavyo.
vi.                Anapokaa anapenda kuweka miguu yake kama x na kisha kubadilisha mara kwa mara. Ule mguu wa juu utakuwa umeelekea kwako nayo ni dalili kwako.
vii.              Msichana anayekupenda atakuwa anapenda kugusa midomo yake (lips) ama kuuma uma au kuchezea glass ya maji au kitu chochote mkononi kuvuta usikivu wako. Pia kuchezea nywele zake au wanaovaa hereni au bangili watazichezea.
viii.            Labda hapa utahitaji X-ray kuangalia hili: anapokuona tu utaona mboni za macho yake zitacheza cheza kuonyesha shauku aliyonayo kwako. Mboni za macho yake zitaisaliti tamaa au shauku yake kwako. Mboni (dilated) zake zinapanuka sana.
ix.                Anapokuona kwa mara ya kwanza ananyanyua Nyusi zake kwa haraka sana kwako. Hata wanaume linatokea ila kwa wasichana ni tendo la haraka zaidi. Amini usiamini ni jambo la hakika kwa mtu unayevutiwa naye siku zote nyusi zako zitainuka na kuanguka kama ishara ya msisimko. Inachukua kiasi cha robo sekunde kucheza kwa kila mtu duniani kote. Kwanini? Kupandisha nyusi kunafungua zaidi macho kupata Mwanga zaidi ili kuona kwa usahihi unachotaka.
x.                  Kukuonyesha kiganja chake cha ndani (wrist) ni aina nyingine kuwa anakupenda.
xi.                Msichana mwenye aibu: kichwa atainamisha chini kisha atakuangalia kupitia kope (eyelashes) zake kwa juu zikiwa zinatazama chini. Halafu anaogopa ama kuwa na wasiwasi zaidi (increasingly Nervous).
xii.               
  1. Msichana anatamani kujua habari za wakati wako ujao utakuwa wapi. Mnapoagana anaweza kukuuliza utasali wapi wiki ijayo? Je utakuja maombi? Wikiendi utaitumia wapi
  2. Zingatia kwamba Msichana anayekimbilia mfanye naye mapenzi anataka kujihakikishia usalama wake kimwili kwako lakini sio kwamba anakupenda kama mtu kamili mwenye heshima zake. Hivyo ikiwa kweli anakupenda hata kubali kulala nawe kwa kuzini.
  3. Msichana anayekupenda ataepuka mara nyingi kula mbele yako. Anatamani sana kukuvutia wewe. Kumbuka wasichana wengi hawajisikii amani dhidi ya mkao wa kula.
  4. Msichana atakuwa ni mtu wa kujihami sana dhidi ya watu wanaotaka kufanya udadisi juu ya mahusiano yako na yeye. Hataki watu wajue hilo haraka.
  5. Msichana atakuwa mgumu kukubalia na jambo lolote unalozungumza vizuri juu ya msichana mwingine.
  6. Msichana atakuwa ni mtu anakueleza mafanikio yake mengi anapohitaji kupata pongezi au sifa kutoka kwako.
  7. Msichana anajenga uadui ama kutopendezwa na wanawake wowote wanaonekana kuwa karibu na wewe. Atakuwa anatumia lugha ya ukali au kujitenga nao.
  8. Msichana atatamani kukutambulisha kwa marafiki zake na pia kukutana na wa kwako.
  9. Msichana atakuwa wazi kukueleza siri zake ambazo hajamwambia mtu yeyote kisha atataka ushauri kutoka kwako. Hiyo ni dalili tosha kuwa anataka urafiki kwako.
  10. Msichana atakuwa anapenda kukualika kwenye sherehe Fulani Fulani ama matukio Fulani ama matembezi maalumu. Usimuhukumu haraka kuwa ana mwenendo mbaya bali msikilize atajifunua kwako. Anaweza hata kutuma marafiki zake ambao aliowatambulisha kwako lakini anaowaamini kukueleza kusudi lake wazi wazi.
  11. Msichana atakuwa anakutazama kwa kuibia mara nyingi unapofanya mambo yake huku akitabasamu ama mnapoachana atakuwa anakuangalia sana na mara unapogeuka bila yeye kutazamia atatabasamu kwa fumanizi hilo.
  12. Wakati msichana anapokuwa na marafiki zake kisha mara unapoingia mahali walipo unakuta wote wananyamaza kimya ama vicheko vya kipumbavu vinakoma na kutaka kuondoka ni dalili kuwa tayari amekiri mbele yao penzi lake kwako.
  13. Msichana anakosa raha na uchangamfu mara anapogundua una jambo linakusibu ama unapougua. Hata na yeye anaugua kwa kukuhurumia wewe. Atatoa taarifa kila mahali juu ya kuumwa kwako. Atahitaji kukusaidia katika tatizo lako.

Kipimo ambacho Mwanaume unaweza kuthibitisha kuwa msichana anakupenda:
  1. Ikiwa unapenda mzaha msichana atapenda kuleta mizaha itakayokufanya ucheke naye lakini akiwa na tahadhari nyingi asije akakukwaza ama kumuona mhuni. Mvulana ili kuthibitisha hili zungumza kitu cha kichekesho mkiwa kikundi cha watu hata kama hakichekeshi sana msichana yule atacheka sana kwa ajili yako. Lakini akitabasamu tu atakuwa anakuhurumia tu.
  2. Msichana anapokuwa amependeza msifie kuwa leo umependeza kweli: ikiwa anakupenda atacheka na hata kukusogelea zaidi kwa kugonga ama kukusukuma kidogo.
  3. Msichana unapojaribu kuongea naye anajisikia aibu sana kuliko wavulana wengine anaowachukulia kama marafiki tu.
  4. Unapowaona marafiki zake wanakusogelea wewe zaidi na yeye anakuwa mbali nawe, tambua ni dalili kuwa huenda amewatuma. Watakuwa wanakuzungumzia habari zake.
  5.  

MAJUKUMU YA MWANAFAMILIA


SEMINA: MAJUKUMU YA MWANAFAMILIA
(Masomo ya Kaya na Familia, Makambi ya 2013: Mtayarishaji: Mkurugenzi wa Vijana, TU)

A.      UTANGULIZI: KWA NINI SEMINA HII IFUNDISHWE KWA WANAFAMILIA?

Semina hii ni ya muhimu kwako kwa sababu mbili kuu. Kwanza changamoto za kimahusiano zinazotokana na jamii ilivyo kwa sasa zinakuhusu, maana huwezi kujiepusha na mambo ya  kijamii. Pili changamoto za kifamilia zimeathiri maisha ya kiroho ya walio wengi, hivyo kujikuta wakimpatia Mungu nafasi ya pili badala ya nafasi ya kwanza. Huwezi kujiepusha na mambo ya kiroho kisha ukafanikisha mambo ya kifamilia. Mambo ya kijamii na mambo ya kiroho yanatakiwa kuunganishwa kwa ustadi ili mwanadanu apate sifa ya kumpendeza Mungu na kuwapendeza wanadamu. Sababu hizi mbili zinafafanuliwa kwa kutumia vipengele vifuatavyo:

            Hoja za kijamii
a.      Hutuwezi kujiondoa katika masuala ya  Kaya na kifamilia
1.      Kwa kuzaliwa  kila mtu huwa ni mtoto katika familia ya wazazi wake.
2.      Kwa kuoa au kuolewa mtu huanzisha familia yake wenyewe bila kutupilia mbali familia ya wazazi wake.
3.      Familia moja huunda ukoo, jamaa na jamuia tunamoishi.
4.      Maadili ya familia moja huunganika na maadili ya familia nyingine na kuitwa maadili ya jumuia.
5.      Itikadi, mazoea  na utamaduni wa  jamuia  ni matokeo ya itikadi  na mazoea  na utamaduni wa kaya/familia  moja moja zikiwekwa pamoja.
6.       Kaya ndiyo muhimili unaoathiri familia na jamii. Ni sahihi pia kusema kuwa  kaya   ndiyo muhimili wa Taifa lolote na muhimili wa Kanisa maana tunaiona jamii katika jicho la kaya moja moja na athari zake.

b.      Kaya na Familia kama jicho la Taifa
1.      Uaminifu katika taifa mzizi wake uko katika uaminifu ndani ya familia
2.      Migogoro ndani ya taifa hueleza migogoro ndani ya familia
3.      Ufisadi, rushwa na dhuluma katika taifa hueleza ufisadi, rushwa na dhuluma katika familia.
4.      Taifa linapojaribiwa kusambaratika/kuvunjika ni taarifa kuwa familia zimetengana au zimevunjika.
5.      Taifa haliwezi kupenda vita endapo familia zilizo ndani yake hazipendi vita, maana waathirika wa vita watakuwa ni wanafamilia.

c.       Kaya na Familia  kama jicho la Kanisa
1.      Waumini wa kanisa wanatoka katika kaya moja moja, ambao hutumika kama matofali ya kujengea Kanisa.
2.      Ubora wa maisha ya kaya/familia moja moja hutangaza ubora wa maisha ya Kanisa
3.      Unachokiona ndani ya familia kitaonekana ndani ya Kanisa
4.      Kisichoonekana ndani ya familia hakitaonekana ndani ya kanisa




d.      Je ni nini kinachotokea katika Familia leo?
1.      Mtazamo kuhusu ndoa unabadilika –kutoka kuwa  AGANO   na kuwa  MKATABA
2.      Mgogoro katika majukumu ya wana ndoa. Yampasayo mume au mke yanapingwa kwa hoja za kimaendeleo- haki sawa kwa wote.
3.      Msongo unaotokana na masuala ya kifedha unazidi kuongezeka miongoni mwa wanafamilia.
4.      Kanuni za ndoa zilizo heshimiwa kiafya zinakataliwa kwa kigezo cha mageuzi ya kimaendeleo.
5.      Mzazi kutokuwa na muda wa kukaa na mtoto anayehitaji malezi yake,(Parenting inadequancy)
6.      Vurugu na magomvi katika familia- mawasiliano kukatika
7.      Familia kuvunjika na kubakia Kaya zilizojitenga
8.      Kasi kubwa ya talaka inayochochea watoto kukosa maskani ya wazazi yanayoeleweka.
9.      Kubomoka kwa mfumo wa kifamilia, kama matokeo ya ongezeko la watoto waliozaliwa nje  ya ndoa.
10.  Maisha ya kukata tamaa, kutengana na hasira
11.  Wazazi kuwatelekeza watoto wao kwa sababu zozote wanazokuwa nazo.
12.  Watoto kutowahudumia wazazi wao kwa vigezo mbalimbali vikwemo wao kujiona ni  wazazi  pia au kujilipiza kisasi kwa vile wao pia walitelekezwa katika makuzi yao.

          Hoja za Kiroho
a)      Kaya na Familia ni changamoto kwa Kanisa
1.      Kwa kuwa nyumbani,(kaya), ndiko chimbuko la tabia, lugha, na mahusiano yote;
2.      Na  kwa kuwa nyumbani,(kaya),kunamfuata mtu kokote aendako, ikiwemo  Kanisani;
3.      Kanisa linalo jukumu maalumu la kuzisaidia kaya na familia ili tabia inayaotakiwa kuonekana kanisani ianzie kuonekana nyumbani.
4.      Utaratibu wa kanisa kupeleka huduma zake nyumbani katika kaya moja moja ni kanuni ya kibiblia na haitakiwi kupuuzwa.
5.      Kabla ya dhambi na baada ya dhambi, Mungu ameonyesha kujishughulisha na mtu mmoja mmoja ndani ya familia, ijapokuwa wakati mwingine hutenda kwa kutumia familia nzima,(Mwanzo 2:16,17; 3:8-19; 4:3-7).

b)      Changamoto za kifamilia zina athari  kwa makuzi ya kiroho.
Familia ya kwanza kabisa, ya Adamu na Hawa, hutufundisha  ubaya wa dhambi na matokeo
yake  yasiyopendeza:
Ø  Rejea na tafakari kisa cha Mwanzo 4:1-8, kumuhusu Kaini Habili na Adamu.
Ø  Wazazi  kuwa  waanzilishi wa matatizo; watoto wakawa ni waathirika wa kwanza kwa makosa ya wazazi wao.
Ø  Maneno  yanayosemwa na  ndugu  katika familia yanaweza kusikika kama mazuri kumbe yana mauaji ndani yake,(mkakati wa Kaini).
Ø  Uaminifu na utiifu kwa Mungu, (mfano wa Habili katika familia  ya Adamu), waweza kuchochea mabaya dhidi ya mhusika, yaliyotendwa na wenzake, bila Mungu kuingilia kati ili kuokoa maisha yake.
Ø  Uhasama miongoni mwa  watoto wa Adamu, uliochochea hasira hadi mauaji ulitokana na matendo ya kidini, yaliyosigana katika msingi wa kiroho.
Ø  Migogoro katika familia nyingi huchochewa na mitizamo au itikadi za kidini zilizo tofauti miongoni mwa wanafamilia, na hasa tendo la ibada.
Ø  Mungu ameruhusu tendo la ibada liwe kiini cha pambano kuu. Je ibada yako inazingatia maagizo ya Mungu au maagizo yaliyo na msingi wa kifamilia tu?

c)      Ujio wa Yesu wa mara ya kwanza ulitanguliwa na mtayarishaji wa njia aliyeandaliwa toka nyumbani ndani ya kaya na familia. Huyu ni Yohana Mbatizaji, (Math3:1-3).
Ø  Je yuko mwanafamilia anayeandaliwa kwa ajili ya kumtengenezea Yesu njia ili awaokoe watu kupitia utume wa familia yenu?
Ø  Kama hayuko mwanafamilia kwa kusudi hilo, je familia nzima ina mpango gani wa kumtambulisha Yesu kwa jamii iliyokosa maadili?
Ø  Ujumbe wa Yohana mbatizaji, yaani Eliya aliyetabiriwa, ulianza kwa kupatanisha familia kwanza,(Luka 1:13-19).
Ø  Ujio wa Yesu wa mara ya pili utanguliwa na  ujumbe wa kupatanisha familia pia,(Malaki 4:5,6)
Ø  Ujumbe wa mwisho kwa ulimwengu huanzia kwa familia kuisikia sauti ya Mungu. Hii ni kwa sababu uovu huanzia kwa mtu mmoja mmoja ndani ya ndoa kwanza kisha ndani ya familia.
Ø  Unabii wa utimilifu wa kujirudia mahusiano ya aina hii umewekwa wazi na Kristo mwenyewe katika Biblia. Rejea Math 24:36-41 juu ya uzoefu wa Nuhu, Lutu na maadili ya zama hizi.

            Nini kifanyike kusaidia changamoto hizi kwa njia ya kanisa?
     Programu  maalumu ya  uamsho na matengenezo yenye lengo la kuzipatanisha familia  kabla ya 
     ujio wa Yesu mara ya pili inatakiwa kuandaliwa na kila kanisa  ili kufanikisha  yafuatayo:

1.      Kuwafundisha wanafamilia jinsi ya kuishi kama watu wanao wajibika kwanza kwa  Mungu, pili kwa familia zao  kila siku.

2.      Kuwasaidia wanafamilia  kupata uelewa wa jinsi ya kukabiliana na changamoto za kimahusiano- mume na mke; mzazi na mtoto, n.k

3.      Kuzisaidia familia jinsi ya kutumika kama vyombo vya kutangaza neema ya Mungu. Hii ni kwa sababu maisha huanzishwa na Mungu na hukomeshwa na Mungu. Kuyajua maagizo ya Mungu ni muhimu maishani.

4.      Ikumbukwe kuwa: ‘familia moja iliyo na nidhamu na utaratibu mzuri, huwa na mvuto wa  nguvu zaidi kwa niaba ya ukristo (kuuelezea ukristo) kuliko mahubiri yote yanayoweza kuhubiriwa’, (Adventist Home uk 32).

5.      Ikumbukwe kuwa: ”Kuwa sehemu ya familia ni rahisi sana; kudumisha uhusiano wa kifamilia ni zoezi gumu. Kuishi kwa furaha katika familia uliyomo bila msaada wa Mungu, inaaminika kuwa ni sanaa inayofikirika.

6.       Endapo kijana hakupewa malezi mazuri na wazazi wake na hivyo hali hiyo kuchangia  tabia mbaya anayoidumisha, hilo halitakuwa ni udhuru mbele za Mungu, maana  ni jukumu lake kusahihisha tabia iliyoharibika maishani mwake bila kutoa udhuru wa kutolelewa vizuri. Hivyo wahusika na malezi ya vijana ni wote: Wazazi, Kanisa kupitia Idara  husika, na Vijana wenyewe. Hoja ni, “Je unafanya nini kutimiza wajibu wako”? Tambua wajibu wako na uutimize.

B.      UWAJIBIKAJI WA KILA  MWANAFAMILIA
Kila mwanafamilia anao uwajibikaji anaodaiwa  kila siku ili kuboresha mahusiano ya kifamilia  ndani ya familia yake na katika jamii aishimo. Tukiyaunganisha mashauri ya Mtume Paulo anayoyatoa katika 1Timotheo 5 na Waefeso 5 na 6, tunapata uwajibikaji wa madaraja manne, kila daraja  na uwajibikaji unaolipasa. Tutafafanua uwajibikaji wa kila daraja miongoni mwa madaraja manne yafuatayo:
1.       Mwana familia kama Mtoto na majukumu yake
2.      Mwanafamilia kama Mzazi na majukumu yake
3.      Mwanafamilia kama Mwenzi na majukumu yake
4.      Familia kama kiungo cha jamii na majukumu yake

C.      MWANA FAMILIA KAMA MTOTO  (MAJUKUMU YAKE)
1.      Je Mtoto ni nani  na ni lini mtu hukoma kuitwa mtoto?
Maana ya neno “mtoto” kibiblia huvuka ile ya kikamusi. Kikamusi mtoto ni mtu mwenye miaka chini ya 18 ya umri. Kibiblia mtoto ni yule anayejielewa kuwa anao wazazi anaowaita “Baba” au “ Mama” kimahusiano, anaotegemewa awahudumie kwa heshima zote,(Kutoka 20:12; Waefeso 6:1-3; 1Timotheo 5:1-4). Katika mtizamo huu utoto wa kifamilia hukoma wazazi wanapoisha kwa kufariki.

2.      Majukumu binafsi yampasayo mtoto mwenyewe?
1)      Mtoto analo jukumu la kutafuta kujua maana ya maisha na kuishi.
2)      Kuwepo duniani kisha mtu asijishughulishe kujua imetokeaje akawepo hapo alipo na makusudi yake, ni udhihirisho wa kutokuwajibika.
3)      Kujitambua yeye ni nani na kusudi lake ni nini huwa miongoni mwa masomo  yaliyo elimu ya msingi katika uwajibikaji wake katika kuishi. Rejea Zaburi 139:13,14.
4)      Kutokuuliza anavyotakiwa kufanya katika kutimiza kusudi la maisha hudhihirisha kutokuwajibika.
3.      Majukumu ya mtoto kwa mzazi
1)      Agenda kubwa huwa ni kuwalipa wazazi wao kihuduma, (1Timotheo 5:1-4)
2)      Jukumu la kuwahudumia wazazi huwa halitolewi udhuru kimahusiano. Mjane hategemewi kutoa udhuru kwa kutokuwahudumia wazazi wake kigezo kikiwa kuwahudumia watoto wake,(1Timotheo 5:1-5). Unapokuwa ni mtoto na ukawa mzazi pia majukumu  huongezeka.
3)      Kwa kuwa mzazi alimlea utotoni, mtoto naye anategemewa amlipe mzazi kwa malezi aliyopewa,(1Timotheo 5:4), hasa pale nguvu zinapokuwa zinazidi kumupungua.
4)      Jukumu maalumu la mtoto analolisema Mfalme Sulemani ni “kumfurahisha mzazi wake”( Mithali 23:24, 25). Kumfurahisha mzazi ni tendo endelevu la kila siku maishani, linalodhihirishwa na kumpa heshima na utii anaositahili kama mzazi,(Kutoka 20:12; Waefeso 6:1-3).
5)      Miongoni mwa matendo yaletayo laana kwa watoto limo hili la kumdharau mzazi wake, (Kumb/Torati 27:16). Kauli hizi zinasisitiza kuwajali wazazi na kuwahudumia muda wote.

4.      Majukumu ya mtoto kwa  wanafamilia na kwa jamii
1)      Yesu ndiye kielelezo cha makuzi na matendo yote ya  maisha.
2)      Katika Luka 2:52 tunaambiwa katika makuzi yake alidumu kumpendeza Mungu na kuwapendeza wanadamu. Wanadamu wanaosemwa hapa sio ndugu zake tu bali ni wote.
3)      Katika 1Timotheo 5:1-3 Mtume Paulo anawaanza vijana na watoto kudhihirisha maisha yenye upendo na huduma kwa wengine wasiokuwa ni ndugu. Asema,” Mzee usimkee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli”.  Hii ni jamii inayoongelewa hapa.
4)      Katika Waraka wa kwanza wa Yohana sura ya pili mafungu ya saba hadi kumi na moja tunaambiwa, ukiishi kwa kumuchukia ndugu yako unakuwa unaishi gizani wala si nuruni tena unakuwa hujui utokako na uendako. Maisha yetu ni lazima yawe na faida kwetu na kwa wengine.
5)      Katika 1Yohana 4:20 tunaambiwa kwamba, “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.”
6)      Unapokuwa ni mtoto miongoni mwa wanafamilia ya wazazi wako, majukumu huongezeka ili kuwahudumia wazazi, ndugu na jamii.


D.      MAJUKUMU YA MWANAFAMILIA KAMA MZAZI
1.      Mzazi ni nani, na ni lini mtu hukoma kuwa mzazi?
1)      Mzazi ni yeyote yule aliyeshiriki tendo la kufanya mtoto azaliwe.
2)      Kwa mujibu wa maana hii ya mzazi, wapo wazazi wanaozaa kihalali na wanaozaa kiharamu.
3)      Iwayo yote, mtu hukoma kuwa mzazi anapkuwa hana watoto wa kulea, au hana watu wanaomwita mzazi.

2.      Majukumu ya Mzazi kwa Mtoto wake
1)      Watoto wawe wamezaliwa kihalali au kiharamu wote huwa  ni watoto wa mzazi, na uwajibikaji wa mzazi kwao unafanana.
2)      1Timotheo 5:7,8 inataja jukumu mojawapo la mzazi kuwa ni utunzaji wa watoto wake.  Tunapozaa na tukakwepa kutunza kunakodhihirishwa na kujali kisha tukimbilie kwa Mungu, hata ibada yetu kwa Mungu huwa haikubaliwi.
3)      Mithali 22:6 inataja jukumu jingine la malezi. Kulea kunakotajwa hapa kunahusisha mafundisho, ambayo hayategemewi kuachwa hat atakapokuwa mzee.
4)      Tunapozaa na kuwa mbali na watoto huwa vigumu kutekeleza malezi yawapasayo. Katika Kumb/Torati 6:4-9 tunaelezwa mazingira tunamolelea watoto: tutembeapo njiani, tuketipo katika nyumba zetu, tulalapo, tuondokapo, tena kwamba ni agizo la Bwana kuwafundisha watoto kwa bidii.
5)      Kwa kifupi majukumu ya mzazi kwa mtoto ni ya aina 6 hivi: Kumfundisha, (Teach), Kumwelekeza, (Train), Kumhudumia katika mahitaji ya maisha, (Provide), Kumuadibisha, (Nurture), Kumtiisha,(control), na  Kumpenda, kumwonyesha upendo), (to love). Kila moja katika haya 6 ni mada inayohitaji mzazi ajifunze jinsi ya kuitekeleza ipasavyo.


3.      Changamoto za majukumu ya kuwa mzazi na jinsi ya kuzikabili
1)      Mtoto anataka muda wa kukaa na kufunzwa na mzazi, wakati mzazi anadhani anataka muda wa kumtafutia mtoto mahitaji.
2)      Kutokukaa na mtoto nyumbani kwa muda wa kutosha ni kushindwa kumfundisha majukumu yafanyikayo nyumbani, hivyo kushindwa kumuandaa kuwa msimamizi wa shughuli za nyumbani kwake anapokuwa mkubwa.
3)      Tabia  na mazoea yote hujengwa katika umri mdogo usiozidi miaka mitano, na hasa ule wa miaka miwili kurudi chini. Kumweka mtoto mbali na mzazi katika kipindi hicho ni kunjengea mazingira yaliyomunyima ujenzi wa tabia au njia impasayo.
4)      Kuwa mtoto kisha uwe mzazi na uwe mwanafamilia utakiwaye kutumika kama ndugu kwa wenzako kunagharimu kuoanisha muda na uwezeshaji.
5)      Kuhangaika ili kutoa huduma za kimwili kwa watoto na hapo hapo uhakikishe huduma za kiroho hazikupungua kwa watoto ndipo udhihirisho wa mzazi anatunza walio wake.
6)      Kitendo cha kuwapeleka watoto wadogo katika shule za bweni ili wapate mzazi mwingine huko ni kukataa jukumu la kulea ukabakiza la kuwa mzazi.
7)      Kutokuwashirikisha watoto malezi ya kiroho kwa kwenda nao katika mikutano ya kidini na kuwahimiza kuishiriki, na kuhakikisha mambo wanayojifunza ni kukosa muda wa kuwafanya watoto wamjue Mungu na kumpenda. Wanaposhindwa kumjua Mungu na kumpenda hawatampenda mzazi kama alivyotazamia hapo wawapo watu wazima.
8)      Kuwazuia watoto wasishiriki katika progarmu za Idara ya vijana zenye lengo la kumsaidia mzazi kuwapatia watoto malezi ya kiroho na kuwaandaa kwa uongozi wa kanisa, ni kuwanyima fursa ya kulipenda kanisa na kumtumikia Mungu kwa njia ya kanisa.
9)      Tunapoamua kusomesha watoto wetu katika shule zisizo za kanisa letu kwa vigezo vyo vyote vile, huwa ni ukubali kuwa makanisa hayo yana elimu na malezi bora kuliko ya kanisa letu. Watakapoharibika kitabia mzazi atabebeshwa hatia ya  mtoto maana amemtengenezea mazingira ya malezi yaliyomuathiri mtoto.
10)  Ikumbukwe kuwa sio rahisi kuondoa madhara ya elimu mbovu aliyopewa mtoto kwa masaa 9 kutwa kwa kutumia dakika 20 za maombi ya nyumbani wakati somo linalojadiliwa halikumlenga yey bali watu wazima.
11)  Haya yote yangetupatia hadhali kuwa tunatakiwa kurekebisha ratiba za utendaji wetu ili kuwa na muda wa kutosha kusadia tabia za watoto wetu ili wapate kuokolewa.

E.        MAJUKUMUYA MWANAFAMILIA KAMA MWENZI  (WANANDOA)

1.      Mume na Mke katika  ndoa wanatambulikaje?
1)      Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, mume na mke hutambulika kwa vigezo kadhaa, miongoni mwake vikiwemo: kuwa na cheti cha ndoa; kuonekana wakiishii ndani ya chumba kimoja kwa kipindi kisichopungua miezi sita hata kama hawana cheti cha ndoa.
2)      Kibiblia mume na mke hutambulika kwa kuwa uchi wote wawili, kama hatua ya kuwa mwili mmoja, (Mwanzo 2:24,25)
2.      Mume na Mke katika ndoa majukumu yao ya msingi ni yapi?
Kusudi la kuwepo mke ni ili awe mwenzi kwa mume, ambaye ni msaidizi wa kufanana naye, (2:18). Je ni nini kinachodhihirisha utendaji wa kuwa mwezi au msaidizi wa kufanana na mwenzake?
1)      Kuishi maisha ya kuambatana wote wawili, (Mwanzo 2:24)
2)      Kuyachanganya ama kayunganisha maisha ya wawili kuwa kitu kimoja,(Kutay/Njia-1 uk.147)
3)      Kuitumikia furaha ya mwenziwe kwa kufurahishana kila mmoja,(Kutay/ Njia-1 uk.143.
4)      Ili majukumu hayo matatu yatekeleze, kunahitajika wasifu au vigezo vingine vinavyoendana ili kuboresha mahusiano hayo. Vigezo hivyo vinaorodheshwa kuanzia no 5 kuendelea.
5)      Anayejiandaa kuwa mume au kuwa mke inabidi ajifunze jinsi ya kujitawala na jinsi ya kuwatendea wengine, (Kutayarisha Njia- 1 uk.145).
6)      Kuunganisha maisha ya wawili kuwa kitu kimoja kunamhitaji kila mmoja kuongeza uvumilivu kwa kutumia uvumilivu,(Kutayarisha Njia-1 uk.147).
7)      Mume aishi kwa kumpenda mkewe kama Kristo anavyolipenda Kanisa, kwa lengo la kulisafisha, akilenga kuwa mwokozi wa mwili badala ya kuunajisi, Waef.5:22-28).
8)      Mke aishi kwa kumtii mumewe katika kila jambo kama Kanisa limtiivyo Kristo, (Waefeso 5:22-24).
9)      Majukumu kuanzia no 5-8 yanawaelekeza wanandoa kutafuta kujua mapenzi ya Mungu yanayofanikishwa na mahusiano ya kindoa. Mashauri ya kuishi kwayo katika ndoa sio yale yatokanyao na mila zetu bali ni yale yatokanayo na Biblia inavyoelekeza.
10)  Ni katika muktadha huu tunapopata jukumu la nyongeza la wanandoa kuwa na muda wa pamoja wa kumwomba Mungu ili awaoneshe watakiwacho kufanya na jinsi ya kukifanya ili kumpendeza Mungu. Changamoto kubwa ya mwanadamu ni,”Kufanya kitakiwacho, kwa wakati utakiwao, na kwa namna itakiwayo”, (Christian Service, EG. White)

F.       MAJUKUMU YA FAMILIA KATIKA JAMII
1.      Familia inayo huduma gani kwa Familia jirani?
Kila mkristo anatgemewa aishi katika jamii akidhihirisha uwajibikaji wa aina mbili, yani kutumika kama chumvi na kama nuru, (Math. 5:13-16). Ufanunuzi wa uwajibikaji huu unaelezwa katika aya zinazofuata.
1)      Familia iishi kwa namna ambayo italeta radha ya kimadili ikilenga familia jirani zijifunze maadili yampendezayo Mungu kutoka kwa familia hiyo.
2)      Familia iishi kwa kuzuia uozo wa kitabia kwa kukemea matendo maovu yanayofanyika katika ujirani wake ili kziambukizza familia zingine kufanya yale yampendezayo Mungu.
3)      Familia iishi kama nuru inayoonesha njia kwa wasioijua njia ya wema na haki  na kweli  ikihimiza familia zingine kufuata kielelezo chake.
4)      Ili kufanikisha uwajibikaji wa aina hii familia haitegemewi iishi katika mazingira ya kujitenga na jamii kwa lengo la kuepuka uovu na dhambi. Inategemewa kuishi kwa kuchangamana na jamii bila kuchanganyika, (Yohana 17:14-18; 1Wakorintho 5:9-13).
5)      Kuishi kwa kuchangamana na jamii ni kulia na wanaolia, kufurahi na wanaofurahi, kuhuzunika na wanohuzumika kwa kuwasaidia katika magumu ynayowaumiza, kisha kuwaalika kumwamini na kumtii Mungu unayeishi kwa kumtumikia.
2.      Maswali muhimu ya kujiuliza
1)      Je familia yako inazo familia rafiki zisizo za waumini wenzako kwa ajili ya uinjilisti?
2)      Je familia yako ina mlango uliofunguliwa kutembelewa na familia jirani kihuduma?
3)      Kama majibu ya maswali haya ni hapana, unahitajika kufanya matengenezo kifamilia.

Nakuthamini

ikiwa kuna jambo lolote zuri lenye kuboresha au kufundisha usisite kuwasiliana nami. Blog hii ni kwa ajili yetu wote kutufundisha na kutuelekeza yatupasayo kutenda kwa maana wakati umekaribia ambapo yeye ajae anakuja na wala hatakawia. Nyosha mapito yako,tambua tabia yako kila mtafute Bwana maana anapatikana nawe ukimwita atakuitikia.