Pages

Friday, 13 June 2014

NAMNA YA KUPATA MWENZI ANAYEKUFAA MAISHANI( PR MWANGA)


NAMNA YA KUPATA MWENZI ANAYEKUFAA MAISHANI

Ndoa iliyo bora na furaha tele haianzi hewani bali ina msingi wake. Furaha siyo kitu cha kupata kama bahati nasibu. Ni jambo ambalo unajenga kama mtu ajengavyo nyumba imara. Lazima aweke msingi ambao utafanya nyumba idumu au ianguke. Hivyo kijana wa kiume na wa kike picha halisi ya ndoa bora na yenye amani inafanyika wakati wa uchaguzi wako wa kupata mwenzi wa maisha yako. Uchaguzi wowote na namna ulivyofanyika utaamua hatima ya aina ya ndoa uitakayo. Zipo kanuni chache tutakazoziangalia kwa vijana wa kike na kiume namna wanavyoweza kupata mwenzi atakayewapa furaha na amani tele katika nyumba zao badala ya majuto na huzuni. Na pia kuondoa kauli laiti ningejua au najuta kuolewa na mwanaume huyu ama kumuoa mwanamke huyu.

MVULANA UTAMPATAJE MSICHANA ATAKAYEKUWA MWENZI ANAYEFAA
Zipo kanuni za msingi ambazo kama kijana wa kiume unaweza kufanya katika uchaguzi wako. Hebu twende hatua kwa hatua katika swala hili:
  1. Kijana mpatie Yesu maisha yako kwa asilimia 100. Jitoe kwa Yesu ili akupe mke mwema. Kumbuka mke mwema hutoka kwa Bwana. MITHALI 31:10.
  2. Maombi ndio silaha na dira itakayokuonyesha chaguo lako. Orodhesha sifa za binti umtakaye awe mwenzi wako. Huenda awe msomi, mfanyakazi, mkulima, mtu wa kiroho, mkarimu, na kadhalika. MWANZO Kisa cha Isaka na Rebeka.
  3. Fanya uchaguzi wa mchumba. Kisha anza kujenga urafiki na pia fanya uchunguzi wa mwenendo wa maisha yake ili upate dalili uzitakazo. Hapa usiharikishe kumtakia kuwa utamuoa maana ataficha makucha yake.
  4. Fanya liwe ni jambo la lazima kuoana na mtu wa imani moja na wewe. Usikubali kuoana na mtu ambaye siyo wa imani moja na wewe. Mkatoliki awe mkatoliki. Mwislamu hali kadhalika. Epuka kugawa watoto na kuondoa furaha na umoja wa familia. Na hata kushindana katika mambo ya imani.
  5. Chukua muda wa kutosha kujifunza tabia yake. Usiharakishe kumuoa bila kujifunza tabia yake. Uchumba wenu usipungue miezi sita na kuendelea. Upande wa pili usizidi sana miaka minne. Muda mfupi haukupatia nafasi ya kujua madhaifu yake na mazuri yake. Muda mrefu nao unaleta mashaka na kujaribiwa kwa mwenzi wako anapoona miaka inasonga hasa mwanamke.
  6. Oana na mwanamke ambaye tabia zenu zinafanana ama kulingana au kuendana. Kama ni mkulima basi usitafute binti wa ofisini yatakushinda.
  7. Kijana epuka kuoa maumbile ya mwanamke (physical appearance). Wengi wanajutia kwani hakujua mwili huwa unachujuka wakati mwanamke anapoolewa aidha kwa kuzaa ama kukabaliana na changamoto za ndoa. Miguu ya bia huwa inabadilika na kuwa ya Coca Cola. Namba nane huwa namba moja.
  8. Usifanye uchaguzi wa sura pekee kama kiini cha chaguo lake. Bali tabia iwe ndicho kiini cha kwanza na sura iwe namba pili. Ni kweli ni vizuri ukaoa mwanamke ambaye ana sura nzuri hata ukitembea barabara unafahari kwenda naye. Siyo ambaye unaona haya kumtambulisha kama mkeo. Lakini sura ikiwa ndicho kiini utaishia kwenye majuta kila siku maana visura wengi bado hawajazaliwa.
  9. Unapopata msichana tafuta ushauri wa watu wenye heshima wanaomfahamu vizuri. Wanaweza kuwa wachungaji, masheikh, wazee au watu wa makamo. 
  10. Epuka msichana mwenye tamaa vitu. Msichana anayekuomba mara hiki au kile huyo atakusumbua mapema.
  11. Jaribu kujua habari za marafiki wa karibu sana wa Yule msichana. Utakapoona na wale ambao hapo mtaani wanasifika kwa tabia mbaya ni dalili mbaya kwa mahusiano yako na yake. Hapa unaweza kumpima kwa kutoka naye out’utakapoona anasimamishwa kila kona tambua kuwa huyo ni jamvi la wageni. Msichana anayejiheshimu huwezi kusimamishwa njia yote na wanaume.
  12. Mwisho: Unapogundua mapungufu ambayo huyapendi ni bora kuvunja uchumba kuliko kuvunja ndoa. Tambua huwezi kumbadilisha mtu tabia yake. JASIRI HAACHI ASILI!

MSICHANA UTAPATAJE MVULANA ANAYEKUFAA MAISHANI MWAKO
Kazi ya ziada kwa msichana kujua mvulana ambaye ni wa kweli. Kwani ni vigumu sana kwa wasichana wengi kujifunza tabia ya kijana wa kiume kwa makini sana. Wasichana wanaona haya kuuliza habari za mvulana Fulani kwa watu kwani wanaogopwa kuulizwa unataka nini kwake. Lakini yapo mambo ya muhimu sana ambayo msichana unaweza kufanya ili kupata mwenzi ambaye atakupa furaha ya kweli katika ndoa yako. Kumbuka mwanamke nawe unauchaguzi wa kufanya. Fanya mambo yafuatayo:
  1. Msichana jitoe maisha yako kwa Yesu kwa asilimia zote ili Bwana akupatie kilicho bora maishani mwako. MITHALI 16:7
  2. Msichana jiheshimu sana mbele za watu na hata uwe mwaminifu mbele ya jamii unayoishi.
  3. Weka swala hili katika maombi na pia weka sifa Fulani ambazo unazitaka kutoka kwa Mungu kwa mwenzi atakayekupatia. Sifa ya kwanza ombea upate mcha Mungu.
  4. Usikatishwe tamaa unapoona vijana wengi hawakufuati. Tulia maana siku zote mambo mazuri hayana haraka. Usipayuke yuke kuwa mbona huolewi.
  5. Chagua mwanaume anayependa kazi. Usibague kazi anayofanya alimradi ni mtu mwenye bidii acha kuangalia uzuri wa kazi yake. Mwenye bidii anaweza kubadilisha maisha katika hali yeyote wakati wowote.
  6. Usikubali kwa gharama iwayo yote kuolewa na mtu ambaye hapendi kazi. Epuka kugeuzwe kuwa kiwanda cha watoto na kuzalishia mali. Epuka kulala njaa na watoto. Ukiolewa na mvuvi nyumba yake itakuwa na taabu nyingi na umasikini mwingi.
  7. Jenga urafiki na wavulana wote kwa heshima. Usibague wavulana wa kuzungumza nao. Wanaume wengi wanaogopwa kudharauliwa na kuaibishwa na wanawake.
  8. Epuka kama ukoma kuolewa mtu asiyeamini au mtu asiye wa imani moja na wewe. Ni vigumu sana kwa wanaume kubadilisha dini yake.
  9. Olewa na mtu mnayefanana tabia zenu. Kama ni mlevi basi olewa na mlevi mwenzako au mvuta sigara mwenzake ili starehe ya  mwingine isiwe kero ya mwingine. Ijapokuwa nyumba ya mlevi kumbuka haina amani. MITHALI 20:1; 23:30 – 35.
  10. Msichana inakupasa uwe ni mtu wa gharama kubwa. Jiweke katika kiwango cha juu hata kama unatoka katika familia masikini. Usikubali kupewa zawadi ovyo ovyo. Kumbuka kila zawadi inayotolewa na mwanaume utailipa.
  11. Usikubali kuolewa na mali au fedha au umaarufu wa mtu. Kumbuka ikiwa utakuwa umefuata hivyo vitu huwa vinayeyuka na matokeo yake upendo wako utayeyuka pia maana ndivyo ulivyofuata hapo. Ni bora kuolewa na masikini anayempenda Mungu kuliko tajiri ambaye hana hofu ya Mungu atakuletea wanawake wengine.
  12. Msichana ni sumu kwa kufanya mapenzi na mvulana unayetaka awe mume wako. Jambo hili litaondoa uaminifu katika ndoa yako na kisha kutakuwa na tabia ya kutokuaminiana siku zote. Ikiwa anakuambia mpaka mfanye kitendo hicho ndipo akuoe ni bora ukavunja uchumba maana kijana huyo sio Mwaminifu kabisa. 

No comments:

Post a Comment

Nakuthamini

ikiwa kuna jambo lolote zuri lenye kuboresha au kufundisha usisite kuwasiliana nami. Blog hii ni kwa ajili yetu wote kutufundisha na kutuelekeza yatupasayo kutenda kwa maana wakati umekaribia ambapo yeye ajae anakuja na wala hatakawia. Nyosha mapito yako,tambua tabia yako kila mtafute Bwana maana anapatikana nawe ukimwita atakuitikia.