Pages

Sunday, 1 June 2014

MAJUKUMU YA MWANAFAMILIA


SEMINA: MAJUKUMU YA MWANAFAMILIA
(Masomo ya Kaya na Familia, Makambi ya 2013: Mtayarishaji: Mkurugenzi wa Vijana, TU)

A.      UTANGULIZI: KWA NINI SEMINA HII IFUNDISHWE KWA WANAFAMILIA?

Semina hii ni ya muhimu kwako kwa sababu mbili kuu. Kwanza changamoto za kimahusiano zinazotokana na jamii ilivyo kwa sasa zinakuhusu, maana huwezi kujiepusha na mambo ya  kijamii. Pili changamoto za kifamilia zimeathiri maisha ya kiroho ya walio wengi, hivyo kujikuta wakimpatia Mungu nafasi ya pili badala ya nafasi ya kwanza. Huwezi kujiepusha na mambo ya kiroho kisha ukafanikisha mambo ya kifamilia. Mambo ya kijamii na mambo ya kiroho yanatakiwa kuunganishwa kwa ustadi ili mwanadanu apate sifa ya kumpendeza Mungu na kuwapendeza wanadamu. Sababu hizi mbili zinafafanuliwa kwa kutumia vipengele vifuatavyo:

            Hoja za kijamii
a.      Hutuwezi kujiondoa katika masuala ya  Kaya na kifamilia
1.      Kwa kuzaliwa  kila mtu huwa ni mtoto katika familia ya wazazi wake.
2.      Kwa kuoa au kuolewa mtu huanzisha familia yake wenyewe bila kutupilia mbali familia ya wazazi wake.
3.      Familia moja huunda ukoo, jamaa na jamuia tunamoishi.
4.      Maadili ya familia moja huunganika na maadili ya familia nyingine na kuitwa maadili ya jumuia.
5.      Itikadi, mazoea  na utamaduni wa  jamuia  ni matokeo ya itikadi  na mazoea  na utamaduni wa kaya/familia  moja moja zikiwekwa pamoja.
6.       Kaya ndiyo muhimili unaoathiri familia na jamii. Ni sahihi pia kusema kuwa  kaya   ndiyo muhimili wa Taifa lolote na muhimili wa Kanisa maana tunaiona jamii katika jicho la kaya moja moja na athari zake.

b.      Kaya na Familia kama jicho la Taifa
1.      Uaminifu katika taifa mzizi wake uko katika uaminifu ndani ya familia
2.      Migogoro ndani ya taifa hueleza migogoro ndani ya familia
3.      Ufisadi, rushwa na dhuluma katika taifa hueleza ufisadi, rushwa na dhuluma katika familia.
4.      Taifa linapojaribiwa kusambaratika/kuvunjika ni taarifa kuwa familia zimetengana au zimevunjika.
5.      Taifa haliwezi kupenda vita endapo familia zilizo ndani yake hazipendi vita, maana waathirika wa vita watakuwa ni wanafamilia.

c.       Kaya na Familia  kama jicho la Kanisa
1.      Waumini wa kanisa wanatoka katika kaya moja moja, ambao hutumika kama matofali ya kujengea Kanisa.
2.      Ubora wa maisha ya kaya/familia moja moja hutangaza ubora wa maisha ya Kanisa
3.      Unachokiona ndani ya familia kitaonekana ndani ya Kanisa
4.      Kisichoonekana ndani ya familia hakitaonekana ndani ya kanisa




d.      Je ni nini kinachotokea katika Familia leo?
1.      Mtazamo kuhusu ndoa unabadilika –kutoka kuwa  AGANO   na kuwa  MKATABA
2.      Mgogoro katika majukumu ya wana ndoa. Yampasayo mume au mke yanapingwa kwa hoja za kimaendeleo- haki sawa kwa wote.
3.      Msongo unaotokana na masuala ya kifedha unazidi kuongezeka miongoni mwa wanafamilia.
4.      Kanuni za ndoa zilizo heshimiwa kiafya zinakataliwa kwa kigezo cha mageuzi ya kimaendeleo.
5.      Mzazi kutokuwa na muda wa kukaa na mtoto anayehitaji malezi yake,(Parenting inadequancy)
6.      Vurugu na magomvi katika familia- mawasiliano kukatika
7.      Familia kuvunjika na kubakia Kaya zilizojitenga
8.      Kasi kubwa ya talaka inayochochea watoto kukosa maskani ya wazazi yanayoeleweka.
9.      Kubomoka kwa mfumo wa kifamilia, kama matokeo ya ongezeko la watoto waliozaliwa nje  ya ndoa.
10.  Maisha ya kukata tamaa, kutengana na hasira
11.  Wazazi kuwatelekeza watoto wao kwa sababu zozote wanazokuwa nazo.
12.  Watoto kutowahudumia wazazi wao kwa vigezo mbalimbali vikwemo wao kujiona ni  wazazi  pia au kujilipiza kisasi kwa vile wao pia walitelekezwa katika makuzi yao.

          Hoja za Kiroho
a)      Kaya na Familia ni changamoto kwa Kanisa
1.      Kwa kuwa nyumbani,(kaya), ndiko chimbuko la tabia, lugha, na mahusiano yote;
2.      Na  kwa kuwa nyumbani,(kaya),kunamfuata mtu kokote aendako, ikiwemo  Kanisani;
3.      Kanisa linalo jukumu maalumu la kuzisaidia kaya na familia ili tabia inayaotakiwa kuonekana kanisani ianzie kuonekana nyumbani.
4.      Utaratibu wa kanisa kupeleka huduma zake nyumbani katika kaya moja moja ni kanuni ya kibiblia na haitakiwi kupuuzwa.
5.      Kabla ya dhambi na baada ya dhambi, Mungu ameonyesha kujishughulisha na mtu mmoja mmoja ndani ya familia, ijapokuwa wakati mwingine hutenda kwa kutumia familia nzima,(Mwanzo 2:16,17; 3:8-19; 4:3-7).

b)      Changamoto za kifamilia zina athari  kwa makuzi ya kiroho.
Familia ya kwanza kabisa, ya Adamu na Hawa, hutufundisha  ubaya wa dhambi na matokeo
yake  yasiyopendeza:
Ø  Rejea na tafakari kisa cha Mwanzo 4:1-8, kumuhusu Kaini Habili na Adamu.
Ø  Wazazi  kuwa  waanzilishi wa matatizo; watoto wakawa ni waathirika wa kwanza kwa makosa ya wazazi wao.
Ø  Maneno  yanayosemwa na  ndugu  katika familia yanaweza kusikika kama mazuri kumbe yana mauaji ndani yake,(mkakati wa Kaini).
Ø  Uaminifu na utiifu kwa Mungu, (mfano wa Habili katika familia  ya Adamu), waweza kuchochea mabaya dhidi ya mhusika, yaliyotendwa na wenzake, bila Mungu kuingilia kati ili kuokoa maisha yake.
Ø  Uhasama miongoni mwa  watoto wa Adamu, uliochochea hasira hadi mauaji ulitokana na matendo ya kidini, yaliyosigana katika msingi wa kiroho.
Ø  Migogoro katika familia nyingi huchochewa na mitizamo au itikadi za kidini zilizo tofauti miongoni mwa wanafamilia, na hasa tendo la ibada.
Ø  Mungu ameruhusu tendo la ibada liwe kiini cha pambano kuu. Je ibada yako inazingatia maagizo ya Mungu au maagizo yaliyo na msingi wa kifamilia tu?

c)      Ujio wa Yesu wa mara ya kwanza ulitanguliwa na mtayarishaji wa njia aliyeandaliwa toka nyumbani ndani ya kaya na familia. Huyu ni Yohana Mbatizaji, (Math3:1-3).
Ø  Je yuko mwanafamilia anayeandaliwa kwa ajili ya kumtengenezea Yesu njia ili awaokoe watu kupitia utume wa familia yenu?
Ø  Kama hayuko mwanafamilia kwa kusudi hilo, je familia nzima ina mpango gani wa kumtambulisha Yesu kwa jamii iliyokosa maadili?
Ø  Ujumbe wa Yohana mbatizaji, yaani Eliya aliyetabiriwa, ulianza kwa kupatanisha familia kwanza,(Luka 1:13-19).
Ø  Ujio wa Yesu wa mara ya pili utanguliwa na  ujumbe wa kupatanisha familia pia,(Malaki 4:5,6)
Ø  Ujumbe wa mwisho kwa ulimwengu huanzia kwa familia kuisikia sauti ya Mungu. Hii ni kwa sababu uovu huanzia kwa mtu mmoja mmoja ndani ya ndoa kwanza kisha ndani ya familia.
Ø  Unabii wa utimilifu wa kujirudia mahusiano ya aina hii umewekwa wazi na Kristo mwenyewe katika Biblia. Rejea Math 24:36-41 juu ya uzoefu wa Nuhu, Lutu na maadili ya zama hizi.

            Nini kifanyike kusaidia changamoto hizi kwa njia ya kanisa?
     Programu  maalumu ya  uamsho na matengenezo yenye lengo la kuzipatanisha familia  kabla ya 
     ujio wa Yesu mara ya pili inatakiwa kuandaliwa na kila kanisa  ili kufanikisha  yafuatayo:

1.      Kuwafundisha wanafamilia jinsi ya kuishi kama watu wanao wajibika kwanza kwa  Mungu, pili kwa familia zao  kila siku.

2.      Kuwasaidia wanafamilia  kupata uelewa wa jinsi ya kukabiliana na changamoto za kimahusiano- mume na mke; mzazi na mtoto, n.k

3.      Kuzisaidia familia jinsi ya kutumika kama vyombo vya kutangaza neema ya Mungu. Hii ni kwa sababu maisha huanzishwa na Mungu na hukomeshwa na Mungu. Kuyajua maagizo ya Mungu ni muhimu maishani.

4.      Ikumbukwe kuwa: ‘familia moja iliyo na nidhamu na utaratibu mzuri, huwa na mvuto wa  nguvu zaidi kwa niaba ya ukristo (kuuelezea ukristo) kuliko mahubiri yote yanayoweza kuhubiriwa’, (Adventist Home uk 32).

5.      Ikumbukwe kuwa: ”Kuwa sehemu ya familia ni rahisi sana; kudumisha uhusiano wa kifamilia ni zoezi gumu. Kuishi kwa furaha katika familia uliyomo bila msaada wa Mungu, inaaminika kuwa ni sanaa inayofikirika.

6.       Endapo kijana hakupewa malezi mazuri na wazazi wake na hivyo hali hiyo kuchangia  tabia mbaya anayoidumisha, hilo halitakuwa ni udhuru mbele za Mungu, maana  ni jukumu lake kusahihisha tabia iliyoharibika maishani mwake bila kutoa udhuru wa kutolelewa vizuri. Hivyo wahusika na malezi ya vijana ni wote: Wazazi, Kanisa kupitia Idara  husika, na Vijana wenyewe. Hoja ni, “Je unafanya nini kutimiza wajibu wako”? Tambua wajibu wako na uutimize.

B.      UWAJIBIKAJI WA KILA  MWANAFAMILIA
Kila mwanafamilia anao uwajibikaji anaodaiwa  kila siku ili kuboresha mahusiano ya kifamilia  ndani ya familia yake na katika jamii aishimo. Tukiyaunganisha mashauri ya Mtume Paulo anayoyatoa katika 1Timotheo 5 na Waefeso 5 na 6, tunapata uwajibikaji wa madaraja manne, kila daraja  na uwajibikaji unaolipasa. Tutafafanua uwajibikaji wa kila daraja miongoni mwa madaraja manne yafuatayo:
1.       Mwana familia kama Mtoto na majukumu yake
2.      Mwanafamilia kama Mzazi na majukumu yake
3.      Mwanafamilia kama Mwenzi na majukumu yake
4.      Familia kama kiungo cha jamii na majukumu yake

C.      MWANA FAMILIA KAMA MTOTO  (MAJUKUMU YAKE)
1.      Je Mtoto ni nani  na ni lini mtu hukoma kuitwa mtoto?
Maana ya neno “mtoto” kibiblia huvuka ile ya kikamusi. Kikamusi mtoto ni mtu mwenye miaka chini ya 18 ya umri. Kibiblia mtoto ni yule anayejielewa kuwa anao wazazi anaowaita “Baba” au “ Mama” kimahusiano, anaotegemewa awahudumie kwa heshima zote,(Kutoka 20:12; Waefeso 6:1-3; 1Timotheo 5:1-4). Katika mtizamo huu utoto wa kifamilia hukoma wazazi wanapoisha kwa kufariki.

2.      Majukumu binafsi yampasayo mtoto mwenyewe?
1)      Mtoto analo jukumu la kutafuta kujua maana ya maisha na kuishi.
2)      Kuwepo duniani kisha mtu asijishughulishe kujua imetokeaje akawepo hapo alipo na makusudi yake, ni udhihirisho wa kutokuwajibika.
3)      Kujitambua yeye ni nani na kusudi lake ni nini huwa miongoni mwa masomo  yaliyo elimu ya msingi katika uwajibikaji wake katika kuishi. Rejea Zaburi 139:13,14.
4)      Kutokuuliza anavyotakiwa kufanya katika kutimiza kusudi la maisha hudhihirisha kutokuwajibika.
3.      Majukumu ya mtoto kwa mzazi
1)      Agenda kubwa huwa ni kuwalipa wazazi wao kihuduma, (1Timotheo 5:1-4)
2)      Jukumu la kuwahudumia wazazi huwa halitolewi udhuru kimahusiano. Mjane hategemewi kutoa udhuru kwa kutokuwahudumia wazazi wake kigezo kikiwa kuwahudumia watoto wake,(1Timotheo 5:1-5). Unapokuwa ni mtoto na ukawa mzazi pia majukumu  huongezeka.
3)      Kwa kuwa mzazi alimlea utotoni, mtoto naye anategemewa amlipe mzazi kwa malezi aliyopewa,(1Timotheo 5:4), hasa pale nguvu zinapokuwa zinazidi kumupungua.
4)      Jukumu maalumu la mtoto analolisema Mfalme Sulemani ni “kumfurahisha mzazi wake”( Mithali 23:24, 25). Kumfurahisha mzazi ni tendo endelevu la kila siku maishani, linalodhihirishwa na kumpa heshima na utii anaositahili kama mzazi,(Kutoka 20:12; Waefeso 6:1-3).
5)      Miongoni mwa matendo yaletayo laana kwa watoto limo hili la kumdharau mzazi wake, (Kumb/Torati 27:16). Kauli hizi zinasisitiza kuwajali wazazi na kuwahudumia muda wote.

4.      Majukumu ya mtoto kwa  wanafamilia na kwa jamii
1)      Yesu ndiye kielelezo cha makuzi na matendo yote ya  maisha.
2)      Katika Luka 2:52 tunaambiwa katika makuzi yake alidumu kumpendeza Mungu na kuwapendeza wanadamu. Wanadamu wanaosemwa hapa sio ndugu zake tu bali ni wote.
3)      Katika 1Timotheo 5:1-3 Mtume Paulo anawaanza vijana na watoto kudhihirisha maisha yenye upendo na huduma kwa wengine wasiokuwa ni ndugu. Asema,” Mzee usimkee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli”.  Hii ni jamii inayoongelewa hapa.
4)      Katika Waraka wa kwanza wa Yohana sura ya pili mafungu ya saba hadi kumi na moja tunaambiwa, ukiishi kwa kumuchukia ndugu yako unakuwa unaishi gizani wala si nuruni tena unakuwa hujui utokako na uendako. Maisha yetu ni lazima yawe na faida kwetu na kwa wengine.
5)      Katika 1Yohana 4:20 tunaambiwa kwamba, “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.”
6)      Unapokuwa ni mtoto miongoni mwa wanafamilia ya wazazi wako, majukumu huongezeka ili kuwahudumia wazazi, ndugu na jamii.


D.      MAJUKUMU YA MWANAFAMILIA KAMA MZAZI
1.      Mzazi ni nani, na ni lini mtu hukoma kuwa mzazi?
1)      Mzazi ni yeyote yule aliyeshiriki tendo la kufanya mtoto azaliwe.
2)      Kwa mujibu wa maana hii ya mzazi, wapo wazazi wanaozaa kihalali na wanaozaa kiharamu.
3)      Iwayo yote, mtu hukoma kuwa mzazi anapkuwa hana watoto wa kulea, au hana watu wanaomwita mzazi.

2.      Majukumu ya Mzazi kwa Mtoto wake
1)      Watoto wawe wamezaliwa kihalali au kiharamu wote huwa  ni watoto wa mzazi, na uwajibikaji wa mzazi kwao unafanana.
2)      1Timotheo 5:7,8 inataja jukumu mojawapo la mzazi kuwa ni utunzaji wa watoto wake.  Tunapozaa na tukakwepa kutunza kunakodhihirishwa na kujali kisha tukimbilie kwa Mungu, hata ibada yetu kwa Mungu huwa haikubaliwi.
3)      Mithali 22:6 inataja jukumu jingine la malezi. Kulea kunakotajwa hapa kunahusisha mafundisho, ambayo hayategemewi kuachwa hat atakapokuwa mzee.
4)      Tunapozaa na kuwa mbali na watoto huwa vigumu kutekeleza malezi yawapasayo. Katika Kumb/Torati 6:4-9 tunaelezwa mazingira tunamolelea watoto: tutembeapo njiani, tuketipo katika nyumba zetu, tulalapo, tuondokapo, tena kwamba ni agizo la Bwana kuwafundisha watoto kwa bidii.
5)      Kwa kifupi majukumu ya mzazi kwa mtoto ni ya aina 6 hivi: Kumfundisha, (Teach), Kumwelekeza, (Train), Kumhudumia katika mahitaji ya maisha, (Provide), Kumuadibisha, (Nurture), Kumtiisha,(control), na  Kumpenda, kumwonyesha upendo), (to love). Kila moja katika haya 6 ni mada inayohitaji mzazi ajifunze jinsi ya kuitekeleza ipasavyo.


3.      Changamoto za majukumu ya kuwa mzazi na jinsi ya kuzikabili
1)      Mtoto anataka muda wa kukaa na kufunzwa na mzazi, wakati mzazi anadhani anataka muda wa kumtafutia mtoto mahitaji.
2)      Kutokukaa na mtoto nyumbani kwa muda wa kutosha ni kushindwa kumfundisha majukumu yafanyikayo nyumbani, hivyo kushindwa kumuandaa kuwa msimamizi wa shughuli za nyumbani kwake anapokuwa mkubwa.
3)      Tabia  na mazoea yote hujengwa katika umri mdogo usiozidi miaka mitano, na hasa ule wa miaka miwili kurudi chini. Kumweka mtoto mbali na mzazi katika kipindi hicho ni kunjengea mazingira yaliyomunyima ujenzi wa tabia au njia impasayo.
4)      Kuwa mtoto kisha uwe mzazi na uwe mwanafamilia utakiwaye kutumika kama ndugu kwa wenzako kunagharimu kuoanisha muda na uwezeshaji.
5)      Kuhangaika ili kutoa huduma za kimwili kwa watoto na hapo hapo uhakikishe huduma za kiroho hazikupungua kwa watoto ndipo udhihirisho wa mzazi anatunza walio wake.
6)      Kitendo cha kuwapeleka watoto wadogo katika shule za bweni ili wapate mzazi mwingine huko ni kukataa jukumu la kulea ukabakiza la kuwa mzazi.
7)      Kutokuwashirikisha watoto malezi ya kiroho kwa kwenda nao katika mikutano ya kidini na kuwahimiza kuishiriki, na kuhakikisha mambo wanayojifunza ni kukosa muda wa kuwafanya watoto wamjue Mungu na kumpenda. Wanaposhindwa kumjua Mungu na kumpenda hawatampenda mzazi kama alivyotazamia hapo wawapo watu wazima.
8)      Kuwazuia watoto wasishiriki katika progarmu za Idara ya vijana zenye lengo la kumsaidia mzazi kuwapatia watoto malezi ya kiroho na kuwaandaa kwa uongozi wa kanisa, ni kuwanyima fursa ya kulipenda kanisa na kumtumikia Mungu kwa njia ya kanisa.
9)      Tunapoamua kusomesha watoto wetu katika shule zisizo za kanisa letu kwa vigezo vyo vyote vile, huwa ni ukubali kuwa makanisa hayo yana elimu na malezi bora kuliko ya kanisa letu. Watakapoharibika kitabia mzazi atabebeshwa hatia ya  mtoto maana amemtengenezea mazingira ya malezi yaliyomuathiri mtoto.
10)  Ikumbukwe kuwa sio rahisi kuondoa madhara ya elimu mbovu aliyopewa mtoto kwa masaa 9 kutwa kwa kutumia dakika 20 za maombi ya nyumbani wakati somo linalojadiliwa halikumlenga yey bali watu wazima.
11)  Haya yote yangetupatia hadhali kuwa tunatakiwa kurekebisha ratiba za utendaji wetu ili kuwa na muda wa kutosha kusadia tabia za watoto wetu ili wapate kuokolewa.

E.        MAJUKUMUYA MWANAFAMILIA KAMA MWENZI  (WANANDOA)

1.      Mume na Mke katika  ndoa wanatambulikaje?
1)      Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, mume na mke hutambulika kwa vigezo kadhaa, miongoni mwake vikiwemo: kuwa na cheti cha ndoa; kuonekana wakiishii ndani ya chumba kimoja kwa kipindi kisichopungua miezi sita hata kama hawana cheti cha ndoa.
2)      Kibiblia mume na mke hutambulika kwa kuwa uchi wote wawili, kama hatua ya kuwa mwili mmoja, (Mwanzo 2:24,25)
2.      Mume na Mke katika ndoa majukumu yao ya msingi ni yapi?
Kusudi la kuwepo mke ni ili awe mwenzi kwa mume, ambaye ni msaidizi wa kufanana naye, (2:18). Je ni nini kinachodhihirisha utendaji wa kuwa mwezi au msaidizi wa kufanana na mwenzake?
1)      Kuishi maisha ya kuambatana wote wawili, (Mwanzo 2:24)
2)      Kuyachanganya ama kayunganisha maisha ya wawili kuwa kitu kimoja,(Kutay/Njia-1 uk.147)
3)      Kuitumikia furaha ya mwenziwe kwa kufurahishana kila mmoja,(Kutay/ Njia-1 uk.143.
4)      Ili majukumu hayo matatu yatekeleze, kunahitajika wasifu au vigezo vingine vinavyoendana ili kuboresha mahusiano hayo. Vigezo hivyo vinaorodheshwa kuanzia no 5 kuendelea.
5)      Anayejiandaa kuwa mume au kuwa mke inabidi ajifunze jinsi ya kujitawala na jinsi ya kuwatendea wengine, (Kutayarisha Njia- 1 uk.145).
6)      Kuunganisha maisha ya wawili kuwa kitu kimoja kunamhitaji kila mmoja kuongeza uvumilivu kwa kutumia uvumilivu,(Kutayarisha Njia-1 uk.147).
7)      Mume aishi kwa kumpenda mkewe kama Kristo anavyolipenda Kanisa, kwa lengo la kulisafisha, akilenga kuwa mwokozi wa mwili badala ya kuunajisi, Waef.5:22-28).
8)      Mke aishi kwa kumtii mumewe katika kila jambo kama Kanisa limtiivyo Kristo, (Waefeso 5:22-24).
9)      Majukumu kuanzia no 5-8 yanawaelekeza wanandoa kutafuta kujua mapenzi ya Mungu yanayofanikishwa na mahusiano ya kindoa. Mashauri ya kuishi kwayo katika ndoa sio yale yatokanyao na mila zetu bali ni yale yatokanayo na Biblia inavyoelekeza.
10)  Ni katika muktadha huu tunapopata jukumu la nyongeza la wanandoa kuwa na muda wa pamoja wa kumwomba Mungu ili awaoneshe watakiwacho kufanya na jinsi ya kukifanya ili kumpendeza Mungu. Changamoto kubwa ya mwanadamu ni,”Kufanya kitakiwacho, kwa wakati utakiwao, na kwa namna itakiwayo”, (Christian Service, EG. White)

F.       MAJUKUMU YA FAMILIA KATIKA JAMII
1.      Familia inayo huduma gani kwa Familia jirani?
Kila mkristo anatgemewa aishi katika jamii akidhihirisha uwajibikaji wa aina mbili, yani kutumika kama chumvi na kama nuru, (Math. 5:13-16). Ufanunuzi wa uwajibikaji huu unaelezwa katika aya zinazofuata.
1)      Familia iishi kwa namna ambayo italeta radha ya kimadili ikilenga familia jirani zijifunze maadili yampendezayo Mungu kutoka kwa familia hiyo.
2)      Familia iishi kwa kuzuia uozo wa kitabia kwa kukemea matendo maovu yanayofanyika katika ujirani wake ili kziambukizza familia zingine kufanya yale yampendezayo Mungu.
3)      Familia iishi kama nuru inayoonesha njia kwa wasioijua njia ya wema na haki  na kweli  ikihimiza familia zingine kufuata kielelezo chake.
4)      Ili kufanikisha uwajibikaji wa aina hii familia haitegemewi iishi katika mazingira ya kujitenga na jamii kwa lengo la kuepuka uovu na dhambi. Inategemewa kuishi kwa kuchangamana na jamii bila kuchanganyika, (Yohana 17:14-18; 1Wakorintho 5:9-13).
5)      Kuishi kwa kuchangamana na jamii ni kulia na wanaolia, kufurahi na wanaofurahi, kuhuzunika na wanohuzumika kwa kuwasaidia katika magumu ynayowaumiza, kisha kuwaalika kumwamini na kumtii Mungu unayeishi kwa kumtumikia.
2.      Maswali muhimu ya kujiuliza
1)      Je familia yako inazo familia rafiki zisizo za waumini wenzako kwa ajili ya uinjilisti?
2)      Je familia yako ina mlango uliofunguliwa kutembelewa na familia jirani kihuduma?
3)      Kama majibu ya maswali haya ni hapana, unahitajika kufanya matengenezo kifamilia.

No comments:

Post a Comment

Nakuthamini

ikiwa kuna jambo lolote zuri lenye kuboresha au kufundisha usisite kuwasiliana nami. Blog hii ni kwa ajili yetu wote kutufundisha na kutuelekeza yatupasayo kutenda kwa maana wakati umekaribia ambapo yeye ajae anakuja na wala hatakawia. Nyosha mapito yako,tambua tabia yako kila mtafute Bwana maana anapatikana nawe ukimwita atakuitikia.